Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin al-Mousawi, Imamu wa Ijumaa wa Baghdad na mwanazuoni mashuhuri wa Hawza ya Najaf al-Ashraf, katika hotuba ya Swala ya Ijumaa ya tarehe 16 Oktoba 2026, alikosoa uamuzi wa viongozi wa Jamhuri ya Azerbaijan wa kupiga marufuku hijabu shuleni, misimamo ya Iraq inayounga mkono upande mmoja dhidi ya wananchi wa Yemen, pamoja na madai ya kugawana nyadhifa za serikali kwa misingi ya kifamilia na kikabila.
Aidha, alitoa wito wa kulinda uhuru wa kidini na kuunda serikali imara nchini Iraq, inayotokana na matakwa ya wananchi, inayozingatia uwezo na sifa za watu katika uteuzi wa viongozi, na inayojitegemea kisiasa.
Katika hotuba yake ya kisiasa, Ayatullah al-Mousawi alisema kuwa; kupiga marufuku wanafunzi na walimu kutumia hijabu ni ukiukaji wa uhuru wa kidini. Alisisitiza kwamba jambo hilo linatia wasiwasi zaidi kwa sababu wananchi wengi wa Jamhuri ya Azerbaijan, licha ya miongo kadhaa ya utawala wa kikomunisti na mapambano dhidi ya dini na alama za kidini, bado wameshikamana na utambulisho wao wa Kiislamu.
Akirejelea msimamo wa ofisi ya Marjaa Mkuu, Ayatullah Sayyid Ali al-Sistani, kuhusu umuhimu wa kushughulikia suala hili, alisisitiza kwamba hijabu inapaswa kuangaliwa kama suala linalohusiana na utamaduni na utambulisho wa jamii, badala ya kulichukulia kuwa ni suala linalohusu matukio machache ya watu binafsi tu.
Ayatullah al-Mousawi pia alitangaza mshikamano wake na wananchi wa Jamhuri ya Azerbaijan na kuwataka wanazuoni, Hawza, Waislamu na wasiokuwa Waislamu kulaani hatua za aina hiyo.
Katika kuendelea na hotuba yake, Imamu wa Ijumaa wa Baghdad alionya kuhusu uwezekano wa kuongezeka vikwazo dhidi ya uhuru wa kidini nchini Iraq. Akizungumzia vizuizi vilivyowekwa dhidi ya safari za mazuwari wa Iraq na nchi nyingine kwa ajili ya kuzuru maeneo matakatifu ya kidini nchini Iran na Iraq, alikosoa kutokuwepo kwa radi amali pana kwa wananchi dhidi ya vikwazo hivyo.
Alisisitiza umuhimu wa kulinda dini, madhehebu na urithi wa kidini, huku akionya dhidi ya kurudiwa ukiukaji wa haki za wanazuoni na vijana wanaoshikamana na dini, kama ilivyotokea katika kipindi cha utawala uliopita nchini Iraq.
Akosoa Msimamo wa Iraq Unaounga Mkono Upande Mmoja Dhidi ya Wananchi wa Yemen
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah al-Mousawi alieleza kuwa mgogoro wa Yemen ni suala linalohusiana na haki na uadilifu. Akikumbusha miaka ya vita na mzingiro dhidi ya nchi hiyo, alisisitiza kwamba matamshi ya viongozi wa Iraq yanayounga mkono misimamo ya Saudi Arabia yanamaanisha kushiriki katika mgogoro huo, badala ya kuwa na msimamo wa kutopendelea upande wowote kidiplomasia.
Akikosoa hatua ya Iraq kujipanga dhidi ya wananchi wa Yemen, alisisitiza kwamba Baghdad hailazimiki kuingilia vita hivyo, lakini haipaswi kuunga mkono upande mmoja dhidi ya mwingine katika mgogoro unaowakabili wananchi wanaokumbwa na mauaji na mzingiro.
Imamu wa Ijumaa wa Baghdad pia alikosoa kutegemea mizania ya nguvu inayobadilika-badilika. Akirejelea maendeleo ya kijeshi yaliyopatikana na harakati ya Ansarullah, alizungumzia kutoridhishwa kwa baadhi ya makundi ya wananchi wa Iraq na msimamo rasmi wa nchi hiyo kuhusu Yemen.
Wakati huohuo, alionya kuhusu matokeo ya sera zinazojengwa juu ya dhuluma na mahesabu ya kisiasa ya muda mfupi.
Maoni yako